Mkuu wa mkoa wa Mtwara, – Gelasius Byakanwa, mkuu wa mkoa wa Kagera,- Brigedia Jenerali Marco Gaguti pamoja na timu ya madereva wa Bodaboda kutoka mikoa hiyo miwili, wametembelea miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali kwenye mkoa wa Dar es salaam.
Katika ziara yao, wakuu hao wa mikoa na madereva hao wa Bodaboda wamemtembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa na jengo la abiria la Tanzanite, mradi wa mabasi ya mwendo wa haraka, ujenzi wa kituo kipya cha mabasi cha Mbezi Luis, daraja la juu la Ubungo na mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi II.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, mkuu wa mkoa wa Mtwara,-Gelasius Byakanwa amesema kuwa wameamua kufuatana na madereva wa Bodaboda kwenye ziara hiyo ili waweze kujionea mambo mazuri na makubwa yanayofanywa na Serikali na wawe mabalozi wazuri kwa wenzao.
Naye mkuu wa mkoa wa Kagera, – Brigedia Jenerali Marco Gaguti ameipongeza Serikali kwa kazi kubwa na nzuri inayoifanya Katika utekelezaji wa miradi yenye lengo la kutatua kero za Wananchi.
Brigedia Jenerali Gaguti amesema mbali na ziara hiyo, tayari walishafanya mashindano ya mpira wa miguu kati ya timu ya Bodaboda Mtwara na timu ya Bodaboda Kagera kwa lengo kujenga uzalendo kwa kundi hilo la vijana na kuwafanya kuwa mabalozi wazuri wa shughuli za Serikali.