Wavunaji mkaa watakiwa kufuata sheria

0
97

Serikali imewataka wananchi wanaofanya biashara ya mkaa kufuata sheria, kanuni na taratibu kwa kuwa kumekuwepo na wimbi la uvunaji wa mazao ya misitu, ukataji na uchomaji wa mkaa bila kufuata sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia biashara hiyo.

Hayo yamesemwa leo Septemba 22,2022 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akijibu swali la Mbunge Nicodemus Maganga wa jimbo la Mbogwe.

Amesema uvunaji holela wa mkaa umesababisha kutoweka kwa kasi kwa maeneo ya misitu na hatimaye kujitokeza kwa athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Kuhusu kauli ya serikali juu ya askari wa misitu wanaowapiga na kuwanyang’anya mkaa wananchi wa Mbogwe Naibu waziri Masanja amesema, wizara ya Maliasili na Utalii haitosita kuwachukulia hatua watumishi wake wanaohusika na uvunjaji huo wa sheria, kanuni na taratibu.

Pia, amewataka wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama wanapotendewa vitendo vibaya na watumishi hao, ili hatua stahiki zichukuliwe.

Akijibu swali la Mbunge wa Tabora Mjini Emmanuel Mwakasaka kuhusu lini serikali itatoa vibali vya uwindaji, Naibu Waziri Mary Masanja amesema vibali vya uwindaji wa kitalii vinaendelea kutolewa kwa mujibu wa kanuni husika ambapo hadi sasa jumla ya minada saba imefanyika na wadau wamepewa vibali vyao.