Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina ameagiza kuondolewa mara moja kwa watumishi wa wanaosimamia kituo cha ukaguzi kilichopo Kibaha mkoani Pwani kwa kushindwa kusimamia rasilimali za sekta ya Mifugo na Uvuvi.
Waziri Mpina ametoa agizo hilo jijini Dodoma wakati wa kikao cha tathmini ya Operesheni Nzagamba awamu ya Pili iliyofanyika kati ya mwezi Oktoba na Novemba mwaka huu kwa lengo la kuinua mchango wa sekta ya mifugo katika pato la Taifa.
Amesisitiza kuwa watumishi wasio waadilfu na wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao hawana nafasi katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ndio maana ameagiza kuondolewa mara moja kwa watumishi wanaofanya kazi ya ukaguzi wa rasilimali katika kituo cha Kibaha.
Hata hivyo Waziri Mpina amewapongeza watumishi wote walioshiriki katika Operesheni Nzagamba awamu ya Pili kwa kufanya kazi kubwa na kwa uzalendo , na kwamba wameonesha kuwa na uwezo wa kusimamia rasilimali za Taifa ili zitoe mchango stahiki katika pato la Taifa.
Waziri huyo wa Mifugo na Uvuvi pia ametumia kikao hicho cha tathmini ya Operesheni Nzagamba awamu ya Pili, kuwaasa Watumishi wa wizara hiyo na wa halmashauri nchini kuhakikisha wanasimamia kwa makini utekelezaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu zote zinazosimamia biashara ya Mifugo na Mazao yake hususani mabadiliko ya Kanuni mpya iliyotolewa mwezi Agosti mwaka huu.