Watumishi watakiwa kupeleka wizara ya Habari kidijitali

0
330

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewataka Watumishi wa wizara hiyo kutambua kuwa wao ni sehemu ya kuipeleka Tanzania kidijitali.

Amesema Watumishi hao wana wajibu, majukumu na dhamana ya kutekeleza sera, sheria, kanuni, miongozo na miradi ya kitaifa ya sekta ya habari, mawasiliano na teknolojia ya habari.

Waziri Nape ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa baraza la Wafanyakazi wa wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, baraza ambalo ni la kwanza kulifungua tangu ateuliwe kuongoza wizara hiyo.

Amewaeleza Wajumbe wa mkutano huo kuwa wao ni kiungo muhimu kati ya menejimenti ya wizara na Wafanyakazi, hivyo ni vema kiungo hicho kusimamiwa vizuri kwa kuwa wizara hiyo inaangaliwa na kufuatiliwa kwa karibu kuliko wizara nyingine kuendana na dhamana ambayo imepewa ya kuipeleka Tanzania kidijitali.

Kwa mujibu wa Waziri Nape, Watumishi hao ni sehemu ya Tanzania inayotakiwa, na kutoa wito kwa Menejimenti ya wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha inaweka mazingira mazuri mahala pa kazi ili Wafanyakazi waweze kutekeleza vema majukumu yao.