Jeshi la polisi mkoa Pwani linawashikilia watumishi saba wa mamlaka ya vitambulisho vya taifa –nchini -NIDA kwa tuhuma za kuiba mali za mamlaka hiyo waliokuwa wakiihamisha kutoka ofisi za zamani zilizoko Tanita kwenda jengo lao jipya lililopo eneo la Loliondo wilayani Kibaha na kwenda kuziuza ,
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa polisi wa mkoa huo Wankyo Nyigesa amesema watuhumiwa hao wamekamatwa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kuwa Polisi waliokuwa doria usiku huo na kutilia shaka gari dogo lililokua likitoka katika ofisi hizo na wakachukuwa hatua ya kulisimamisha na kufanya upekuzi na likakutwa na jenereta moja ya mamlaka hiyo iliyokuwa imeibiwa.
Amesema baada watuhumiwa hao kukamatwa na kupekuliwa katika nyumba wanazoishi walikutwa na mali mbalimbali za NIDA ikiwemo komputa mpakato mbili, boksi mbili zenye vitambulisho vya utaifa elfu kumi na tano pamoja na mali nyingine zote zenye thamani ya shilingi milioni kumi na tano.
Kamanda Wankyo amesema polisi inaendelea kuwahoji watuhumiwa hao na watafikishwa mahakamani taratibu zitakapokamilika.
Katika hatua nyingine Kamanda Wankyo amesema jeshi hilo pia limewakamata watu 29 mkoani humo kwa tuhuma za wizi na uvunjaji wa nyumba katika eneo la Chalinze mkoani humo.
Baadhi ya watuhumiwa hao walikutwa na mali mbalimbali za wizi walizokuwa wamezificha katika handaki moja na dawa za kulevya aina ya bangi, pombe ya gongo na pikipiki moja waliokuwa wakitumia katika matukio ya uporaji.