Watumishi 266 wapandishwa madaraja Babati

0
151

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Deo Ndejembi amesema,, watumishi wa umma nchini wana deni kwa Rais Samia Suluhu Hassan la kufanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu kwani kwa kipindi cha mwaka mmoja Rais ameonesha kujali maslahi yao.

Ndejembi ametoa kauli hiyo alipofanya ziara katika halmashauri ya Babati Mji mkoani Manyara kwa lengo la kuzungumza na watumishi wa umma na kusikiliza kero pamoja na changamoto zinazowakabili.

” Watumishi wa umma tuna deni kubwa kwa Rais Samia, ndani ya muda mfupi wa uongozi wake kapandisha maslahi ya watumishi kwa kuongeza mshahara, kapandisha madaraja tumeona na posho pia zimeongezeka, hii inaonesha jinsi gani alivyo na mapenzi na sisi watumishi,” amesema Ndejembi

Amesema ndani ya muda mfupi serikali imelipa madeni ya watumishi mfano halmashauri ya Mji Babati watumishi 358 wamelipwa malimbikizo ya mishahara yao ambayo ni zaidi ya shilingi milioni 371 na ndani ya mwaka wa fedha 2021/2022 watumishi 266 wamepanda madaraja.

Ndejembi amesema litakua jambo la ajabu kuona watumishi wa umma wanaendekeza vitendo vya rushwa ilihali Serikali imewaboreshea maslahi yao na kwamba hawatosita kumchukulia hatua mtumishi yeyote ambaye atakosa uadilifu kazini.