Watu Wanne wanaotuhumiwa kuwa ni Majambazi, wameuawa katika majibizano ya risasi baina yao na askari wa Jeshi la Polisi nchini wilayani Biharamulo mkoani Kagera.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Jeshi la Polisi nchini imeeleza kuwa, tukio hilo limetokea hii leo katika barabara ya Ngazi Saba inayounganisha nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi, wakati operesheni yenye lengo kupambana na vitendo vya uhalifu ikiendelea katika mikoa ya Geita, Kigoma na Kagera.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa, wakiwa katika doria kwenye maeneo ya barabara hiyo ya Ngazi Saba, askari wa kikosi maalum cha kupambana na uhalifu nchini, wakiongozwa na Kamishina wa Operesheni na Mafunzo kutoka Jeshi la Polisi Liberatus Sabas waliona kundi la watu likikimbilia porini na ndipo waliwaamuru wasimame.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hata baada ya kuamriwa wasimame, watu hao walikataa na kuanza kuwarushia askari risasi na ndipo askari nao waliamua kujibu kwa kurusha risasi na hivyo kusababisha vifo.
Kufuatia tukio hilo, Kamishna huyo wa Operesheni na Mafunzo kutoka Jeshi la Polisi Nchini, -Liberatus Sabas, amewataka Wakazi wa mkoa wa Kagera wanaojua Watoto ama ndugu zao wanajihusisha na vitendo vya uhalifu wajitokeze kutambua miili ya watuhumiwa hao wa Ujambazi, ambayo hivi sasa imehifadhiwa katika hospitali ya mkoa huo.