Watuhumiwa wa ujambazi wauawa Kagera

0
163

Watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wenye umri wa miaka kati ya 25 na 30 wameuawa katika majibizano ya risasi na polisi mkoani Kagera.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kagera, William Mwampaghale amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo na kusema kuwa tukio hilo limetokea katika maeneo ya barabara ya Kumunazi kwenda Relenge wilaya ya Ngara.

Amesema polisi walipata taarifa ya siri kwamba kuna kikundi cha waharifu kimepanga kufanya uharifu kwa kutumia silaha katika maeneo ya Kumunazi na watatumia usafiri wa pikipiki, hivyo waliandaa mtego katika barabara zote zinazoingia Kumunazi.

Kwa mujibu wa Kamanda Mwampaghale, ilipofika majira ya saa tatu na nusu usiku katika maeneo ya barabara ya Kumunazi kwenda Rulenge ilitokea pikipiki iliyokuwa imebeba watu watatu hivyo askari waliokuwa doria katika barabara hiyo walijaribu kuisimamisha lakini walikaidi na kugeuza kurudi walikotoka ndipo walipoanza majibizano ya risasi.

Watuhumiwa hao wa ujambazi waliouawa wamekutwa na bunduki moja aina ya AK 47, risasi 25 na mabomu mawili ya kurusha kwa mkono.

Miili ya watu hao imehifadhiwa katika hospitali ya Nyamiyaga wilayani Ngara kwa ajili ya kutambuliwa na kwa uchunguzi zaidi.