Msako wa nyumba kwa nyumba uliofanywa katika wilaya za mkoa wa Tabora, umewezesha watoto wengi ambao walikuwa hawajaripoti shuleni kufanya hivyo.
Mkuu wa mkoa wa Tabora, Dkt. Batilda Burian amesema mkoa huo uliamua kufanya msako huo baada ya kubaini kuwa watoto wengi wenye sifa hawajaripoti shuleni na walikuwa wakifanya shughuli mbalimbali.
Dkt. Buriani alikuwa akitoa salamu za mkoa wa Tabora mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa hafla ya uzinduzi wa barabara ya Nyahua hadi Chanya yenye urefu wa kilomita 85.4 iliyojengwa kwa kiwango cha lami.
Amesema jitihada za kuwatafuta watoto wengine ili nao waripoti shuleni zinaendelea.
Mkuu huyo wa mkoa wa Tabora ameishukuru serikali kwa kujenga barabara hiyo na kuongeza kuwa tayari wakazi wa mkoa huo wameanza kuonja matunda ya barabara hiyo ya Nyahua hadi Chaya.
Pia amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uzinduzi wa filamu ya Tanzania The Royal Tour ambayo imeitambulisha nchi kimataifa na ambayo imetangaza vivutio vingi vya za utalii na uwekezaji unaoweza kufanyika Tanzania.