Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es salaam kwa kushirikiana na mradi wa Little Hearts wa nchini Saudi Arabia ambao ni moja ya miradi ya Afya iliyo ndani ya Taasisi ya Msaada ya Muntada yenye makao Makuu yake mjini London nchini Uingereza, wamefanya matibabu ya moyo kwa watoto 72.
Matibabu hayo yamefanyika katika kambi maalum ya siku Saba ya matibabu ya moyo kwa watoto wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni pamoja na matundu na mishipa ya damu ya moyo kutopitisha damu vizuri.
Katika kambi hiyo iliyoanza Disemba Mosi mwaka huu, kati ya watoto 72 waliopatiwa matibabu, 43 wamefanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua na 29 wamefanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na hali zao zinaendelea vizuri.
Taarifa iliyotolewa na Taasisi hiyo ya Moyo Jakaya Kikwete imesema kuwa madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wamefanya upasuaji huo kwa kurekebisha valvu, kuziba matundu, kurekebisha mishipa ya moyo ambayo imekaa vibaya na kurekebisha mfumo wa uzungukaji wa damu katika moyo.
Taarifa hiyo imewataka wazazi na walezi nchini kupima afya za watoto wao pale watakapoona kuna hali ya tofauti katika ukuaji wao kwa kuwa magonjwa mengi ya moyo yanaanzia utotoni.