Watendaji wasio waadilifu Jeshi la Polisi kuchukuliwa hatua

0
248

Rais John Magufuli ameliagiza Jeshi la Polisi Nchini, kuwachukulia hatua Watendaji wa Jeshi hilo ambao wamekua wakifanya vitendo kinyume na maadili na kulichafua jeshi hilo.

Akizungumza mara baada ya kuweka  jiwe la msingi la ujenzi wa  nyumba 118 za askari  zilizopo eneo la Nzuguni mkoani Dodoma, Rais Magufuli amesema kuwa,  Jeshi hilo limekua likifanya kazi nzuri, lakini kuna baadhi ya Watendaji ambao wamekua wakifanya vitendo viovu na kulipaka matope, hivyo ni lazima Watendaji wa aina hiyo wachukuliwe hatua.

Amelipongeza Jeshi la Polisi Nchini kwa kuendelea kufanya kazi nzuri licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili, na kuongeza kuwa Serikali kwa upande wake itaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazolikabili Jeshi hilo.

Awali akizungumza kabla ya uwekaji wa jiwe hilo la Msingi, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, – Simon Sirro alieleza kuwa,  ujenzi wa nyumba hizo 118 za askari Polisi katika eneo la Nzuguni utakamilika mwishoni mwa mwaka huu.