Rais John Magufuli amewataka Watendaji wa Kata nchini kutatua kero zinazowakabili Wananchi kwenye maeneo yao, badala ya kusubiri wabebe wabango wakati wa ziara za viongozi.
Rais Magufuli pia amewataka Watendaji hao kutambua kero zinazowakabili Wananchi na kuzitafutia ufumbuzi kwa haraka na kama zikiwashinda waziwasilishe kwa Wakurugenzi wa Halmashauri ili zipatiwe ufumbuzi kwa haraka.
Akizungumza na Watendaji wa Kata zote hapa nchini katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es salaam, Rais Magufuli amewasisitiza watendaji hao kuwatumikia Wananchi na hasa wanyonge katika maeneo yao.
Amewataka Watendaji hao kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika kata zao, ili miradi hiyo iweze kuwa na tija kwa Wananchi wanyonge.
Aidha Rais Magufuli amewataka Watendaji wa Kata zilizopo maeneo ya mipakani kuhakikisha wanasimamia wageni wanaoingia katika kata hizo kutoka nchi jirani na pia kuhakikisha wageni wote wanafuata utaratibu wa kisheria wa kuingia hapa nchini.
Katika hotuba hiyo Rais Magufuli amewataka Watendaji hao kuhakikisha wanajiepusha na vitendo vya rushwa katika kutekeleza majukumu yao, na kutowanyanyasa Wananchi kwa kuwadai rushwa pindi wanapofuata huduma katika ofisi zao.