Watanzania watonywa fursa ughaibuni

0
5313

Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mahmoud Thabit Kombo amewataka Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo nchini humo, kwani kuna fursa lukuki.

Akizungumza mkoani Dar es Salaam katika Jukwaa la Biashara baina ya Tanzania na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) Balozi Kombo amesema, Italia ina uhitaji wa kahawa, hivyo ni vema Watanzania wakachangamkia fursa hiyo ya soko.

Amesema kila mwaka mashirika makubwa ya kahawa duniani hukutana nchini Italia kwa ajili ya kushindanisha bidhaa hiyo na kahawa kutoka Tanzania ndiyo inayoonekana kuhitajika zaidi.

Bidhaa nyingine kutoka Tanzania zenye uhitaji mkubwa katika soko nchini Italia ni Pareto, ngozi na matunda.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Caroline Kitaba, amewataka watanzania kuchangamkia fursa katika sekta ya kilimo kwa kuzalisha mbegu zenye ubora na kwa wingi kwa ajili ya soko la nchi hiyo.

Amesema mbegu nyingi zinazalishwa hapa Tanzania lakini soko lake ni Uholanzi, hivyo watanzania wachangamkie fursa hiyo.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Samwel Shelukindo amesema, kwa sasa soko ni kubwa la mafuta ya Alizeti nchini humo na kwamba soko hilo linahitaji mafuta kutoka Tanzania.