Watanzania watakiwa kuwa Waumini wazuri wa dini zao

0
333

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa, madhehebu ya dini nchini yamekua yakitoa mchango mkubwa katika kuwapata Viongozi wa Serikali wanaofuata maadili mema na miiko ya uongozi.

Akizungumza  wakati wa ufunguzi wa Msikiti wa Haq – Kionga uliopo Magomeni jijini Dar es salaam, Waziri Mkuu Majaliwa amesema imedhihirika kuwa Waumini wazuri wa dini mbalimbali ndio wanakua Viongozi wazuri na waadilifu ndani ya Serikali.

Amewasihi viongozi wa dini nchini kuendelea kuwafundisha maadili mema Waumini wao, ili Taifa liendelee kuwa na Raia wema ambao baadhi yao ndio watakuwa Viongozi katika ngazi mbalimbali hapo baadaye. 
 
“Nyumba za ibada ndiyo mahali sahihi panapojengwa maadili mema kwa watu wa rika zote, nawaomba Watanzania wawe Waumini wazuri wa dini zao kwani kwa kufanya hivyo watakuwa pia ni Raia wema,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Ameongeza kuwa, Wazazi na Walezi nchini wana wajibu wa kuwarithisha watoto wao imani za dini vizuri, kwani anaamini kwa kufanya hivyo watoto watajengewa misingi mizuri ya imani ya dini na maadili mema na watakapokuwa watu wazima watakuwa ni raia wema.

Akiwa katika msikiti huo wa Haq – Kionga, Waziri Mkuu Majaliwa amewasilisha mchango wa Rais John Magufuli wa Shilingi Milioni Kumi na yeye mwenyewe amechangia Shilingi Milioni Tano ili zisaidie katika awamu ya Pili ujenzi wa msikiti huo.