Watanzania watakiwa kuchangia damu

0
187

Meneja wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama Dkt Magdalena Lyimo  amesema kuwa, mpango huo umefanikiwa kukusanya zaidi ya chupa  Elfu 51 ambazo ni sawa  na asilimia Ishirini zaidi ya malengo uliojiwekea kwa mwaka 2018/2019.

Dkt Lyimo ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati akiwasilisha mada ya upatikanaji wa damu,  kwenye kikao kazi cha Waganga Wakuu wa mikoa pamoja na wale wa Halmashauri, na kuongeza kuwa kiasi hicho cha damu kimekusanywa katika kipindi cha kuanzia Julai Mosi hadi hivi sasa.

Amesema kuwa kwa mwaka 2018/2019,  Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama imejiwekea lengo ya kukusanya chupa 309, 376 nchi nzima,  ikilinganishwa na chupa 257, 557 zilizokusanywa mwaka 2017/2018.

Dkt Lyimo amewashukuru Watanzania wote wanaoendelea kuchangia damu, wakiwemo Vijana Watumishi wa Umma, Taasisi pamoja na wale wa Mashirika, na kuwataka wengine kuendelea kujitokeza ili kuchangia damu.