Watanzania wasisitizwa kujituma kufanyakazi

0
1113

Rais John Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili kujiletea maendeleo na kuacha kusubiri serikali ili iwapelekee maendeleo.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa daraja  jipya la Selander litakalounganisha eneo la hospitali ya Aga Khan na Coco Beach kupitia baharini.

Amesema kuwa daraja hilo linajengwa kwa fedha za serikali pamoja na mkopo nafuu kutoka Korea Kusini, nchi ambayo raia wake wamekua wakifanya kazi kwa bidii kubwa na kujituma.

Rais Magufuli pia ametumia hafla hiyo kuwataka Watanzania kuendelea kulinda amani ya nchi kwa kwa kuwa bila nchi kuwa na amani miradi yote ya maendeleo haitaweza kutekelezwa.

 

Amemtaka mkandarasi anayejenga daraja hilo ambaye ni kampuni ya  GSE kutoka Korea Kusini kukamilisha kazi hiyo ndani ya kipindi cha miezi 30 iliyopangwa ama ikiwezekana hata kufupisha muda wa kufanya kazi hiyo.

Ameelezea matumaini yake kuwa kampuni hiyo itafanya kazi kwa ufanisi mkubwa, kutoka na Korea ya Kusini kuwa na Wakandarasi waliobobea kwenye ujenzi wa miundomninu hasa madaraja na barabara.

Kwa upande wake Balozi wa Korea Kusini nchini, –  Cho Tae-Ick amesema kuwa licha ya kuwa ujenzi huo utarahisisha usafiri jijini Dar es salaam pia utaimarisha uhusiano wa Tanzania na nchi hiyo.

 

Daraja hilo jipya la Selander ambalo ni kubwa kwa urefu nchini, litakapokamilika litakua na uwezo wa kupitisha zaidi ya magari elfu 50 kwa siku na hivyo kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es salaam.