Watanzania washauriwa kufungua kampuni za Bima

0
162

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji amewashauri Watanzania ambao wamepata elimu ya Bima kufungua Kampuni za Bima za ndani, ili ziweze kuingia katika ushindani na kampuni za nje.
 
Dkt Kijaji ametoa ushauri huo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa kikao cha Wadau cha kujadili na kutoa maoni kuhusu rasimu ya Mpango Mkuu wa Taifa wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa kipindi cha miaka Kumi kuanzia mwaka 2019/2020 hadi mwaka 2029/2030.
 
Amesema kuwa, kampuni za Bima nchini ni 31 na kati ya hizo za Kitanzania hazidi Tatu, kwa hiyo kuna  kazi kubwa ya kufanya ili vijana waliopata elimu kwenye eneo la Bima waweze kuanzisha kampuni za Kitanzania  na kuwa na ushindani.
 
Naibu Waziri huyo wa Fedha na Mipango ameongeza kuwa, Serikali imeendelea kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano ambao ulianza mwaka 2016/2017 na unaelekea kukamilika mwaka 2020/2021.
 
“Dhima ya mpango huu ni uchumi wa Viwanda, lakini tusiwaache Watanzania nje ya uchumi huu na miongoni  mwa vipaumbele ni kuondoa umasikini wa kipato kwa watu, uimara wa sekta ya fedha ndio nyenzo muhimu ya uimara wa Sekta ya viwanda”, amesisitiza Dkt Kijaji.
 
Amewataka Washiriki wa kikao hicho cha uboreshaji wa rasimu ya Mpango wa Sekta Ndogo ya Fedha kujadili na kutoa maoni kwa weledi, maoni yatakayosaidia kuwa na sekta ya fedha iliyo endelevu na himilivu kwa ukuaji wa uchumi na kuchangia kupunguza umaskini wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.