Watanzania wamkumbuka Sokoine

0
482

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Augustine Mahiga amewataka vijana na viongozi nchini kumuenzi aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Hayati Edward Moringe Sokoine kwa kujifunza uzalendo, uvumilivu, uwajibika na uadilifu.

Waziri Mahiga ameyasema hayo  Monduli mkoani Arusha wakati wa Ibada maalum ya kumbukizi ya miaka 35 ya kifo Sokoine.

Dkt Mahiga amesema kuwa Hayati Sokoine alikuwa ni kiongozi wa mfano kutokana na uwajibikaji na uchapakazi wake  bila kuchoka.

Amewataka vijana wa sasa kutafuta na kujifunza namna ya kumfahamu Edward Moringe Sokoine, lengo likiwa ni kujiongezea elimu bila kuchoka kama alivyopenda kiongozi huyo aliyedaiwa kuwa licha ya kuwa na majukumu mengi hakuacha kuendelea kujifunza.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda amesema kuwa Hayati Sokoine alifanya kazi kubwa ya kuhakikisha kunakuwepo na haki na usawa kwa Watanzania wote  huku  mtoto wa Hayati Sokoine, Balozi Joseph Sokoine  akisema kuwa familia imeanzisha Taasisi ya kusaidia watu wenye uhitaji ambapo kwa mwaka huu wameanza kutoa huduma ya Bima ya Afya kwa watu Mia Sita.