Mwenyekiti wa Kamati ya Maonesho Kitaifa wa Shirika la Uzalishaji Mali Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT), Kanali Shija Lupi ametoa wito kwa Watanzania kuthamini na kuzipenda bidhaa zinazozalishwa nchini na Watanzania.
Ametoa wito huo wakati akitoa tathmini ya ushiriki wao katika Maonesho ya 46 ya Biashara Kimataifa maarufu Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Amesema shirika limeipa kipaumbele suala la ubora katika uzalishaji wa bidhaa zake kusudi ziweze kukidhi vigezo vya ubora na kuwafaa Watanzania wote.
Sambamba na hilo, amesema anaona utofauti mkubwa katika maonesho ya mwaka huu kwani wananchi wameonesha kupenda na kuvutiwa na bidhaa zao akitoa mfano wa bidhaa za samani.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Mstaafu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi wa Serikali ya awamu ya pili, Dkt. George Mlinga amesema shirika hilo limejipambanua vyema katika kuimarisha uchumi wa nchi huku akiongeza kuwa mbali na ulinzi, shirika hilo limefanikiwa kujikita katika shughuli za uzalishaji mali ili kuimarisha uchumi wa taifa.
Leo ni siku ya 14 ya maonesho hayo yanayotarajiwa kuhitimishwa Julai 13, 2022