Watano wapandishwa kizimbani

0
213

Watu watano wamepandishwa kizimbani katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam, wakikabiliwa na mashtaka 14 ikiwemo kosa la uhujumu uchumi na kutakatisha fedha zaidi ya shilingi milioni 300 mali ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
 
Watuhumiwa hao wamesomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali Mkuu Martenus Marandu mbele ya Hakimu Mwandamizi wa mahakama hiyo Rashid Chaungu.
 
Miongoni mwa makosa yaliyotajwa katika kesi hiyo namba 96 ya mwaka 2020 inayomkabili Reginald Masawe na wenzake ni pamoja na kughushi nyaraka mbalimbali ikiwemo leseni ya biashara, hati ya mlipa kodi na kufungua akaunti katika Benki ya NMB kwa kutumia jina la mtumishi wa TANESCO Riziki Kayenga, kosa ambalo wanadaiwa kulitenda kwa nyakati tofauti mwaka 2019 na 2020 jijini Dar es salaam.
 
Aidha katika kosa la kutakatisha fedha, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kushirikiana kutakatisha fedha na kujipatia zaidi ya shilingi milioni 300 mali ya TANESCO wakati wakijua fedha hizo ni matokeo ya makosa ya kiuhalifu.
 
Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka bila kutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi, Wakili wa Serikali Mkuu Marandu amedai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
 
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Disemba 21 mwaka huu na washtakiwa wamerudishwa rumande.