Watano kizimbani kwa kuisababishia TANESCO hasara ya milioni 6

0
356

Watu watano wa wakazi wa Ukonga, jijini Dar es Salaam wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kulisababishia hasara Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Washitakiwa hao ni Mwalimu Boniphace Singaille, Twalibu Kasamu, Mwarami Mussa, Vumilia Kambi na Haidary Hassan

Washitakiwa hao wamesomewa mashitaka yao na Wakili wa Serikali Mkuu, Martenus Marando akisaidianaia na Kija Luzungana, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Kassian Matembele.

Akiwasomea hati ya mashitaka, Wakili Marando amedai kuwa washitakiwa hao kwa pamoja na wenzao wawili ambao ni wagonjwa wanadaiwa Januari 2018 eneo la Kichangani, Ukonga Madafu jijini Dar es Salaam waliingilia miundombinu ya umeme inayotumika kutoa huduma muhimu kwa kung’oa mita ya TANESCO kutoka katika kiboksi kinachohifadhia mita hiyo na kuisababishia TANESCO hasara ya zaidi ya shilingi milioni 6.

Upande wa mashitaka ulidai upelelezi haujakamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Matembele ameema kosa hilo linadhamini kwani thamani ya mali wanayodaiwa washitakiwa hao kuisababishia hasara Tanesco ni chini ya shilingi milioni 10.

Akitaja masharti ya dhamana, Hakimu Matembele ameema kila mshitakiwa anatakiwa kuwa na mdhamini moja anayetambuliwa kisheria, atakayesaini bondi ya shilingi milioni 1.

Hata hivyo washtakiwa hao wamerudishwa rumande baada ya kushindwa kutumiza masharti ya dhamana na kesi hiyo itatajwa tena, Desemba 16, 2020.

Mwisho.