Mkuu wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi nchini Naibu Kamishna Liberatus Sabas amewaomba wakazi wa kijiji cha Masuguru mkoani Mtwara kuwatambua wageni wanaoingia kijijini hapo wakitokea maeneo mbalimbali ya nchi na hata nchi jirani ya Msumbiji.
Naibu Kamishna Sabas amesema kuwa amelazimika kutoa ombi baada ya kubainika kuwa asilimia 90 ya silaha zilizopatikana kufuatia operesheni iliyofanyika mkoani Mtwara kupatikana katika kijiji hicho.
Ametumia mkutano huo kuwaonya watu wote ambao wamekua wakifanya vitendo vya uhalifu na kukimbilia nchi jirani ya Msumbiji ambako huko pia wamekua wakijiunga na vikundi vya uhalifu.
Mkuu huyo wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi Nchini Naibu Kamishna Liberatus Sabas amebainisha kuwa kwa sasa kuna ushirikiano baina ya Tanzania na Msumbiji katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu, hivyo mhalifu anaweza kukamatwa kwa urahisi katika pande hizo mbili.