Watakiwa kutatua kero za wananchi

0
2323

Rais John Magufuli amewaagiza viongozi wa wizara, mikoa na wilaya nchini kuhakikisha kero na malalamiko ya wananchi wanyonge yanatafutiwa ufumbuzi haraka.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi akiwa njiani kutoka Mugumu kwenda Tarime katika eneo la daraja la mto Mara Wilayani Serengeti, na Nyamongo, Nyamwaga na Tarime Mjini Wilayani Tarime ambako ameendelea na ziara yake mkoani Mara.

Kabla ya kutoa agizo hilo Rais Magufuli amekagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la mto Mara lililopo katika barabara inayounganisha Mugumu na Tarime ambalo lina urefu wa mita 94, upana wa mita 9.9 ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 75 na litagharimu shilingi Bilioni 8.5 hadi kukamilika kwake.

Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa daraja hilo, Rais Magufuli amesikiliza kilio cha mama mmoja Nyambura Nyamarasa aliyedai mazao yake yameliwa na mifugo, na kwamba juhudi za kufuatilia haki yake hazijafanikiwa huku akiendelea kuhangaika.

Rais Magufuli ameelezea kutofurahishwa na Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu ambaye hajachukua hatua licha ya mama huyo kumpelekea kilio chake na ameagiza vyombo vya dola vimkamate mtu anayedaiwa kulisha mifugo katika shamba la mama huyo na kumfikisha katika vyombo vya sheria.

“Viongozi niliowachagua na mnaofanya kazi na Serikali ninayoongoza, nataka kuona mnashughulikia matatizo ya watu wanyonge, sitaki kuona watu wenye fedha wanawanyanyasa masikini, na kweli leo nilitaka kukufukuza kazi Mkuu wa Wilaya, nakusamehe lakini kashughulikie haki ya huyo Mama na viongozi wote hakikisheni watu wanyonge hawanyanyaswi” amesema Rais Magufuli.

Katika Mji wa Nyamongo, wananchi wamemuomba Rais Magufuli awasaidie kutatua tatizo la maji huku wakibainisha kuwa kuna fedha shilingi Milioni 700 za mradi huo zimetumika ilihali maji hakuna, pia wamemuomba awasaidie kulipwa fidia waliopisha uwekezaji wa mgodi wa madini.

Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, -Apoo Tindwa amesema kuwa mradi wa maji wa shilingi Milioni 700 unatekelezwa na mwekezaji ambaye ni kampuni ya Acacia na kwamba halmashauri ya wilaya ya Tarime hawajaupokea kutokana na kutotoa maji.

Kuhusu madai ya kulipwa fidia ya ardhi kwa wananchi waliopisha uwekezaji wa kampuni ya madini ya Acacia, Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko amesema kuwa zoezi hilo linakwamishwa na wananchi wenyewe kutokana na baadhi yao kupeleka madai wakati hawana maeneo huku akibainisha kuwa uhakiki uliofanywa na Wizara kwa majina 1,544 umebaini kuwa majina 720 yalikuwa hewa na majina 1,116 wahusika hawakujitokeza kuhakikiwa wakiwemo watumishi wa umma, hivyo akatoa wito kwa wananchi wanaowakwamisha wenzao kulipwa fidia waache kufanya hivyo.

Akizungumza na wananchi wa Nyamongo, Rais Magufuli amesema kuwa atafuatilia utekelezaji wa mradi wa maji unaogharamiwa na kampuni ya Acacia, lakini amewaagiza viongozi wa Tarime na mkoa wa Mara kumfuatilia mtu anayedaiwa kukusanya asilimia moja ya mapato ya mgodi wa Acacia badala ya malipo hayo kupatiwa vijiji sita vinavyozungumza mgodi huo ili aeleze fedha zote alizokusanya na zipo wapi.

“Mnaweza mkawa mnabishana na kupoteza muda kwa ajili ya hizo shilingi Milioni 700 wakati hapa kuna mtu anakusanya fedha nyingi zaidi kwa kujifanya yeye ni mbia kwa niaba ya vijiji sita, hizo fedha anazokusanya zingemaliza matatizo yote ya maji hapa Nyamongo na zingesaidia mahitaji mengine ya wananchi” amesisitiza Rais Magufuli.

Kabla ya kuondoka Nyamongo. Rais Magufuli amesikiliza maombi ya kupatiwa vitabu, mabweni na maabara kutoka kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Ingwe na papo hapo akaendesha harambee ya kuchangisha fedha ambapo amefanikiwa kupata shilingi Milioni 26 zikiwemo shilingi Milioni 5 alizotoa yeye papo hapo kwa ajili ya kusaidia shule hiyo.

Rais Magufuli pia amesalimiana na wakazi wa Nyamwaga ambao wameiomba serikali ihamishie Makao Makuu ya halmashauri ya wilaya ya Tarime Mjini hapo, na katika majibu yake amesema ombi hilo lifikishwe kwake kupitia hatua zinazostahili.

Aidha, Rais Magufuli amehutubia mkutano wa hadhara Mjini Tarime na kuwahakikishia wananchi wa mji huo kuwa serikali itaendelea kuwahudumia wananchi bila kuwabagua na kwamba kwa Tarime imetenga shilingi Bilioni 14 kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji, imeanza ujenzi wa barabara ya Tarime – Mugumu kwa kiwango cha lami, imetoa shilingi milioni 400 za ujenzi wa kituo cha afya, inatoa fedha za elimu bila malipo kila mwezi na inaendelea kusambaza umeme kwa vijiji vyote visivyo na umeme.

Tarehe Nane Septemba, Rais Magufuli anaendelea na ziara yake katika Kanda ya Ziwa kwa kuutembelea mkoa wa Simiyu.