Watakiwa kuhifadhi historia ya nchi kwa usahihi

0
490

Wahifadhi wa Makumbusho na Malikale nchini wameshauriwa kutumia mfumo sahihi katika kuweka taarifa za mikusanyo ili  kusaidia kuendelea kupatikana taarifa sahihi kuhusu urithi wa Tanzania pamoja na historia yake.
 
Wito huo umetolewa mkoani Dar es Salaam na mkuu wa Idara ya Historia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam  Dkt Hezron Kangalawe, alipokuwa akifungua rasmi warsha kuhusu Usajili na Uwekaji sahihi wa kumbukumbu ya mikusanyo iliyopo Makumbusho.
 
Ameongeza kuwa, warsha hiyo itakuwa ni msaada mkubwa hasa wa kuweka kumbukumbu vizuri juu ya mikusanyo iliyopo nchini na ile iliyochukuliwa kipindi cha ukoloni hasa iliyopo nchini Ujerumani.  
 
Kwa upande wake mratibu mkuu wa warsha hiyo Dkt. Oswad Masabo amesema kuwa kuna changamoto katika uhifadhi sahihi wa taarifa za mikusanyo ya kimakumbusho,  hivyo wameona ni muhimu kutoa elimu kwa wahifadhi hasa kupitia wataalam wakongwe ili uhifadhi sahihi na endelevu ufanyike kwa faida ya kizazi kilichopo na kijacho.
 
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Mawazo Ramadhan amesema warsha hiyo itasaidia wahifadhi chipukizi wa taasisi hiyo kuweka sawa taarifa za mikusanyo iliyopo kwenye makumbusho zote nchini.
 
Warsha ya usajili na uwekaji sahihi wa kumbukumbu ya mikusanyo iliyopo Makumbusho ni matokeo ya programu ya utafiti shirikishi wa umahiri inayoendeshwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Makumbusho ya Mila na Desturi ya Berlin, Chuo Kikuu cha Humboldt cha Berlin Ujerumani pamoja na Makumbusho ya Taifa nchini.