Watakaoficha vyakula kushtakiwa

0
200

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeonya kuwachukulia hatua kali ikiwemo kuwafungulia kesi za uhujumu uchumi, wafanyabiashara watakaobainika kwa makusudi kuficha vyakula na bidhaa kwa lengo la kuwapandishia bei wananchi.

Onyo hilo limetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi wakati wa mkutano wake wa kila mwisho wa mwezi na wahariri na waandishi wa habari, Ikulu Zanzibar.

Amesema kuelekea mwezi Mtukufu wa Ramadhani siku chache zijazo, serikali imejihakikishia kuwepo kwa bidhaa nyingi ikiwemo vyakula kama unga wa ngano, mafuta ya kupikia, sukari na mchele ili kukidhi mahitaji ya mfungo wa Ramadhani.

Dkt. Mwinyi amesema serikali haitarajii kuibuka kwa mfumuko wa bei ama bidhaa kuadimika, hali itakayosababisha taharuki kwa wananchi na waumini wa dini ya Kiislamu ambao watakuwa wakitekeleza ibada ya Swaumu.

“Atakayeficha vyakula tutamshitaki kwa kosa la uhujumu uchumi, tumetaarifiwa mchele upo, sukari ipo, ngano ipo na mafuta ya kupikia yapo kwa ajili ya Ramadhani, tukikubaini umehodhi kwa lengo binafsi tutakushitaki kwa kosa la uhujumu uchumi.” ameonya Rais Mwinyi