Wataalamu watakiwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya misitu na nyuki

0
179

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka wataalamu wa masuala ya misitu na nyuki kuangalia namna bora ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya misitu hapa nchini.

Mama Samia ameyasema hayo, wakati wa uzinduzi wa Kongamano la kimataifa la Sayansi linalojadili namna bora ya kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya Misitu na nyuki .

Akisoma hotuba ya ufunguzi wa kongamano hilo kwa niaba ya Makamu wa Rais, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro amesema, licha ya jitihada za kuongeza uzalishaji wa mazao ya misitu na nyuki hapa nchini lakini bado uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mazao ya Nyuki ni mdogo.

Kuhusiana na utunzaji wa mazingira na upandaji miti hapa nchini, Makamu wa Rais ameagiza kila Halmashauri kuhakikisha inapanda miti milioni 1.5 kwa mwaka ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wake Naibu waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amewakumbusha wadau wa Misitu na Nyuki kuhakikisha wanaendeleza sekta hiyo kwa manufaa ya watanzania wanaowekeza katika sekta hiyo.

Nae Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya utafiti wa Misitu Tanzania –(TAFORI) Dkt. Revocatus Mushumbusi amesema kuwa lengo la kongamano hilo ni kujadili kwa pamoja njia za kuendeleza sekta ya misitu na nyuki hapa nchini.

Kongamano hilo pia limeshuhudiwa kuzinduliwa kwa mpango wa kwanza wa Ufugaji Nyuki na mpango wa Tatu wa uendelezaji wa sekta ya misitu hapa nchini.