Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es salaam linawashikilia watu Wanne waliokuwa wafanyakazi wa kampuni ya ulinzi ya G4S kwa tuhuma za wizi wa Shilingi Bilioni Moja na Milioni 336, ambazo ni fedha za Kitanzania na za kigeni.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam,- Lazaro Mambosasa amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Christopher Rugemalila, Salum Shamte, Mohamed Ramadhani na Ibrahim Maunga ambao tarehe Saba mwezi huu walikabidhiwa fedha hizo kutoka matawi ya benki ya NBC Kariakoo na Samora jijini Dar es salaam ili wazipeleke makao makuu ya Benki hiyo yaliyopo posta ya zamani -Sokoine Drive.
Kamanda Mambosasa amesema kuwa, badala ya kuzipeleka fedha hizo sehemu husika watuhumiwa hao waliziiba na kisha kutelekeza gari walilokuwa wakizishafirishia aina ya Nissan Hard Body lenye namba za usajili T728 BAN pamoja na bunduki na bastola.
Amesema mtuhumiwa Christopher Rugemalila mkazi wa Chanika amekamatwa akiwa na Shilingi Milioni 110, Dola Elfu 19 za Kimarekani pamoja na magari madogo matano ambayo ameyanunua kwa kutumia fedha hizo za wizi.
Kamanda Mambosasa amesema kuwa, watuhumiwa Salum Shamte na Mohamed Ramadhani wamekamatwa huko Mbagala na kukutwa na Shilingi Milioni 332 na Dola Elfu 50 za Kimarekani pamoja na viwanja viwili vyenye thamani ya Shilingi Milioni 25.
Mtuhumiwa Ibrahim Maunga amekamatwa na zaidi ya Shilingi Milioni 195, Dola Elfu 70 za Kimarekani, nyumba aliyoinunua Kibaha mkoani Pwani yenye thamani ya Shilingi Milioni 30 na samani zenye thamani ya Shilingi Milioni 10 .
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam pia limewakamata polisi Tisa wakiongozwa na afisa msaidizi wa Polisi kwa tuhuma za kujipatia fedha kutoka kwa Watuhumiwa hao ambao walipaswa kuwakamata lakini walishindwa kufanya hivyo.
Kufuatia tukio hilo, Kamanda Mambosasa ametoa wito kwa kampuni za ulinzi kuajiri wafanyakazi waaminifu ili kuepuka matukio ya wizi kama hayo.
