Watanzania washauriwa kusoma vitabu

0
629

Watanzania wameshauriwa kujenga utamaduni wa kusoma vitabu mbalimbali vya Kiswahili ili kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili.

Ushauri huo umetolewa jijini Dar es salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako wakati wa uzinduzi wa machapisho mapya ya Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), uzinduzi uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

Profesa Ndalichako amesisitiza kuwa ili kukuza lugha ya Kiswahili, Watanzania hawana budi kusoma vitabu mbalimbali vya Kiswahili vilivyoandikwa na watu wenye ujuzi na lugha hiyo.

Mwakilishi wa Waandishi wa habari katika uzinduzi huo ambaye ni miongoni mwa waandishi wa vitabu vinavyozinduliwa ni Victor Eliah kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), ambaye amesema kuwa vyombo vya habari nchini vina nafasi kubwa ya kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Profesa Willium Anangisye ametoa wito kwa wanafunzi na Watanzania wote kujenga tabia ya kusoma vitabu huku Mkurugenzi wa TATAKI, -Dkt Ernesta Mosha akisema kuwa pamoja na machapisho yaliyopo, bado wanaendelea kuandaa machapisho mengine.

Taasisi ya Taaluma za Kiswahili imezindua machapisho mapya Kumi na majarida matatu yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili.