Wasanii wa filamu Mkoani Mtwara wameeleza kufurahishwa na kitendo cha Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Dunstan Kyobya kugharamia vitambulisho kutoka Bodi ya Filamu Tanzania ambavyo vitawezesha wasanii hao kufanya kazi zao kwa amani na uhuru zaidi.
Wakizungumza mara baada ya kukabidhiwa vitambulisho hivyo, wasanii hao wamesema vitawasaidia kutambulika ndani na nje ya nchi kwa sanaa yao wanayofanya kwa ajili ya kutambulisha utamaduni, mila, desturi pamoja na vivutio vya mkoa wa Mtwara kwa Tanzania na nchi nyingine.
“Kipekee kabisa tunashukuru, hiki kitendo kimetufurahisha na kutudhihirishia kuwa viongozi wetu wanatambua umuhimu wa kazi yetu katika kujenga mkoa na nchi yetu kupitia sanaa,” amesema Ratifa Mkali, mwigizaji.