Waokolewa baada ya kufukiwa na kifusi kwa siku 9

0
137

Wachimbaji wawili wa madini ya dhahabu katika
mgodi wa Igalula wilayani Nyang’hwale mkoani Geita
wameokolewa wakiwa hai baada ya kufukiwa na kifusi kwa muda wa siku tisa.

Mmoja wa wachimbaji hao ametambuliwa kwa jina la Prima Shokolo ambaye ndugu yake Francisco Misungwi mkazi Sengerema, Mwanza amesema waliweka matanga kwa siku tatu baada ya kupata taarifa ya ndugu yao kufukiwa na kifusi.

Prima amesema baada ya kukaa kwa muda mrefu walikuwa wamekata tamaa na kuanza kunywa mkojo ili waendelee kuishi, lakini baada ya muda akawa anapoteza fahamu kutokana na njaa kali.

Mchimbaji mwingine Leonatus Nenge amesema walipokuwa ndani ya kifusi hali iliendeleaa kuwa mbaya na walichokuwa wanakifanya ni kumuomba Mungu.

“Nilimwambia Mungu kama umekuja kutuchukua kwa njia hii hapana, naomba usikaushe koo langu ili nitoke humu shimoni.” Amesema Leonatus.

Leonatus na Prima walifukiwa na kifusi Agosti 02, 2023 wakiwa katika shughuli zao za kila siku za kujitafutia riziki katika mgodi wa dhahabu wa Igalula na kwa sasa wanapatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Nyang’hwale.