Wanawake watakiwa kujitokeza uwekezaji sekta ya madini

0
320

Kamishna wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo amewataka wanawake nchini kujitokeza kwa wingi kwenye uwekezaji Sekta ya Madini kutokana na uwepo wa fursa mbalimbali kwenye sekta hiyo kuanzia uchimbaji, uchenjuaji, biashara ya madini na utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini.

Lekashingo ameyasema hayo kupitia kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa mubashara kupitia TBC1 leo 08 Oktoba, 2022 kwenye Maonesho ya Tano ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini katika Viwanja vya Bombambili mjini Geita.

Lekashingo amesema ili kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na sekta ya madini, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuweka kanuni za ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini ili wananchi waweze kupata fursa za ajira na kutoa huduma mbalimbali za kijamii
 
Katika hatua nyingine, amewataka Watanzania kuanzisha viwanda vya kutengeneza vipuri na huduma za usafiri kwenye migodi ya madini, biashara ambayo itakuwa ni endelevu hata mara baada ya kumalizika kwa uchimbaji wa madini.
 
“Zipo kampuni zinazomilikiwa na Watanzania kama Blue Coast kwa ajili ya kutoa huduma za vifaa na usafiri kwenye migodi ya madini, mfano ambao ni mzuri; Tunaomba wadau wengi zaidi kujitokeza ili kunufaika kwa kuwa na biashara endelevu,” amesisitiza Lekashingo.
 
Awali akielezea maonesho hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Profesa Godius Kahyarara amesema kuwa yamekuwa na mafanikio makubwa kwani yametumika kama fursa  kwa kampuni kubwa za uchimbaji wa madini kutoa elimu ya teknolojia mpya ya uchimbaji wa madini na wananchi wengi kupata elimu kuhusu taratibu za kupata leseni za uchimbaji na biashara ya madini kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini.