Washindi wa Tuzo za Mwanamke Kinara kutoka Mikoa 6 ya Kanda ya Ziwa wametembelea Bunge, kwa lengo la kujitambulisha kwa Spika Dkt. Tulia Ackson, Serikali pamoja na kujionea shughuli mbalimbali zinazoendelea Bungeni Jijini Dodoma. Leo Aprili 22, 2022.
Tuzo za Mwanamke Kinara Kanda ya ziwa hutolewa kila Mwaka katika Maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani zenye lengo la kutambua na kuthamini mchango wa Mwanamke katika Jamii na uchumi kwa ujumla, kuhamasisha wanawake katika kujitoa katika jamii na kuinua hali zao za kiuchumi.
Washindi hawa ni kutoka sekta 16 ambazo ni sekta ya elimu, afya, madini, mfanyabiashara biashara bora wa mwaka, mfanyabiashara chipukizi, biashara ya upishi, Upambaji kwenye sherehe, upishi wa keki, habari, ustawi wa jamii, uchumi wa ziwa Victoria, mshehereshaji bora, ufundi nguo, Urembo na Utanashati, kikundi bora cha Wanawake, na Getrude Mongella Tuzo ya Heshima.
Aidha, Washindi hawa wamepata fursa ya kusalimiana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na viongozi mbalimbali katika viwanja vya Bunge.
Tuzo za Mwanamke Kinara zinahusisha Mikoa 6 ya Kanda ya Ziwa Mwanza, Shinyanga, Mara, Kagera, Geita na Simiyu.