Wanataaluma kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo

0
221

Katibu Mkuu wa wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt. Francis Michael amesema wataalamu na wadau wa sekta ya elimu wanapaswa kuandaa mitaala mipya na kuanza kutoa elimu bobezi, ili watahiniwa wapate ujuzi na kuweza kujiajiri bila kusubiri kuajiriwa.

Dkt. Michael ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kongamano la kumbukizi ya miaka 23 tangu kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Amesema kwa upande wa Serikali inaendelea kuandaa mazingira mazuri ya kutoa elimu ya kujitegemea kwa wanafunzi wanaohitimu elimu ya juu, ili kupunguza idadi ya wahitimu wanaotegemea kuajiriwa na Serikali peke yake.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo wa wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kila mwaka idadi ya wahitimu inaongezeka na kwamba serikali haina uwezo wa kuajiri wahitimu wote.

Kwa upande wake mkuu wa chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Profesa Shadrack Mwakalila amesema, chuo hicho kimeamua kupambana na adui ujinga kupitia tafiti ili kumuenzi Hayati Baba wa Taifa kwa vitendo.

Amesema wajibu wa wanataaluma ni kumuenzi mwalimu Nyerere kwa kutimiza wajibu wao katika mapambano dhidi ya maadui watatu ambao ni umasikini, ujinga na malazi.

Profesa Mwakalila amesema viongozi waliofuata baada ya Hayati Baba wa Taifa wameonesha juhudi za kukabiliana na maadui hao lakini bado kuna haja kwa wanataaluma na Watanzania wote kuwaenzi waasisi wa Taifa la Tanzania kwa kuwa wazalendo na wawajibikaji.