Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita, -Hamim Gwiyama kufanya operesheni katika kila kijiji wilayani humo ili kuwabaini watu waliowapa wanafunzi ujauzito na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake wilayani Nyang’hwale baada ya kusomewa taarifa iliyoonyesha kuwa wanafunzi wengi wa kike wamekua wakikatisha masomo yao baada ya kupata ujauzito.
Akizungumza na wakazi wa wilaya hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Sabasaba, Waziri Mkuu Majaliwa ameelezea kusikitishwa na vitendo vya wanafunzi wa kike kupata ujauzito huku wahusika wakiachwa bila ya kuchukuliwa hatua yoyote.
Amesisitiza kuwa serikali haiwezi kulifumbia macho jambo hilo na kuwataka wakazi wa wilaya ya Nyang’hwale kushirikiana katika kuwalinda watoto wao wa kike ili wasipate ujauzito na kwamba serikali itawachukulia hatua watendaji wote nchini ambao katika maeneo yao watoto wa kike watabainika kuwa na ujauzito.
Wanafunzi 72 wamepata ujauzito katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2016 hadi 2018 wilayani Nyang’hwale mkoani Geita .