Wanaovuruga amani kuchukuliwa hatua

0
586

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa  serikali haitasita kumchukulia hatua mtu yeyote  bila kujali cheo, dini ama chama chake atakayejaribu kuvuruga amani, umoja  na mshikamano wa Taifa.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati akifungua  Kongamano la Maadhimisho ya Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere linalofanyika katika Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Ametoa wito kwa Watanzania wote kulinda  amani, umoja na mshikamano  wa Taifa uliopo, kwani ni mambo yaliyosisitizwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere  wakati wa uhai wake na kwa kuyalinda mambo hayo Watanzania watakua wamemuenzi kwa vitendo.

Kwa upande wa Chuo  hicho cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa kina jukumu la kuhakikisha wahitimu wake wanakua Wazalendo, Waadilifu na Wachapakazi mahali pote wanapokua.

Kuhusu ombi la Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere la kutaka chuo hicho kipandishwe hadhi na kuwa Chuo Kikuu, Waziri Mkuu Majaliwa amemuagiza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako afanyiwe kazi jambo hilo kwa kuwa linawezekana.