Wananchi watakiwa kumuenzi Mwl. Nyerere kwa kulinda misitu

0
523

Katika kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mw. Julius Nyerere wadau wa mazingira na utalii nchini wametakiwa kutunza hifadhi za misitu kama sehemu ya kuhamasisha vivutio vya utalii vinavyopatika katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Rai hiyo imetolewa mkoani Pwani na Afisa Misitu Mkuu Kanda ya Mashariki, Shaban Kiula wakati wa maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 21 ya kifo cha kiongozi huyo yaliyofanyika Kinyanyiko, mkoani Pwani.

“Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alikuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha jamii inahifadhi na kutunza misitu ambayo nayo ni chanzo cha uhai wa viumbe mbalimbali,” amesema Kiula.

Kwa upande wake mwakilishi wa Meneja wa Misitu Kanda ya Mashariki, Jane Mwaisambe na baadhi ya wadau wa mazingira na utalii waliotembelea hifadhi ya msitu huo wamesema matembezi hayo yatasaidia kutangaza mazuri ya baba wa taifa kwa vizazi vijavyo.

“Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Jilius Kambarage Nyerere alikuwa mzalendo wa kweli katika kuhamasisha jamii kulinda na kuhifadhi mazingira.”

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na wadau wengine wa mazingira na utalii wameadhimisha kumbukizi ya kifo cha Mwl. Nyerere kwa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo ndani ya hifadhi ya Msitu ya Pugu-Kazimzumbwi.

Vivutio vilivyotembelewa ni pamoja na bwawa la Minaki, Milele cha Msolo na mapango ya mizimu ya Mavuga.