Wananchi katika Mikoa ya Simiyu, Mara na
Shinyanga wamepongeza na kufurahia huduma zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya (NHIF) katika maonesho ya Wakulima yanayofanyika Kitaifa mkoani
Simiyu.
Huduma hizo ni pamoja na Usajili wa Wanachama, elimu juu ya huduma za
matibabu, upimaji wa afya bure na elimu ya kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha
Sandai Wilayani Bariadi Bw. Elisha Nkubira wamesema kuwa huduma zinazotolewa na
Mfuko zimewalenga wananchi wote wakiwemo wa kipato kikubwa na kipato kidogo.
“Huu Mfuko unafanya kazi kubwa sana na hizi huduma ambazo wanazitoa kwenye viwanja hivi hakika ni za mfano wa kuigwa na zimelenga kutusaidia Sisi wananchi ili tujue hali za Afya zetu na kuweza kujikinga na maradhi,” amesema Bw. Nkubira.
Naye Mkazi wa Bunda Bw. Lameck Mwita ambaye pia ni mwanachama wa Mfuko alitoa wito kwa wananchi wengine kuchukua hatua ya kujiunga na huduma za NHIF ili kuwa na uhakika wa kupata matibabu wakati wote.
Amesema kuwa kitendo cha familia kuwa na kadi za matibabu za NHIF ni kinga kubwa ya kuepukana na umasikini kutokana na ukweli kwamba maradhi huja bila taarifa na gharama zake ni kubwa.
Story by. James Range