Wanafunzi washauriwa kwenda kujifunza TAEC

0
144

Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imewashauri  Wanafunzi  wa vyuo Vikuu na shule za sekondari nchini  kutembelea maabara za Tume hiyo, ili kupata mafunzo kwa vitendo juu ya matumizi ya  teknolojia ya nyuklia hapa nchini.

Ushauri huo umetolewa jijini Arusha na Mkuu wa Mafunzo na Utafiti kutoka TAEC Dkt Shovi Sawe, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku moja kwa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Abdul -:Rahman Al-Sumatt cha Zanzibar kuhusu mtambo wa X-ray Fluorescence (XRF) na Gamma Ray Spectroscopy, ikiwa ni sehemu ya mafunzo ya somo la fizikia ya nyuklia.

“TAEC tuna vifaa na watalaam  katika maeneo mbalimbali ya mionzi na nyuklia, hivyo Wanafunzi wanashauriwa kuja kujifunza kwa vitendo,” amesema Dkt Sawe.

Amesema TAEC itaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuongeza uelewa juu ya mionzi,  matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia,  madhara ya mionzi na namna ya kujilinda na madhara hayo.