Wanafunzi 7,400 kushiriki UMITASHUMTA na UMISSETA

0
297

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa leo Juni 8, 2021 anatarajiwa kuzindua Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) , hafla inayofanyika katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe alisema kuwa wanafunzi 7,400 wanatarajiwa kushiriki mashindano hayo ambayo pia hutumika kama njia ya kukuza vipaji vya washiriki.

“Jumla ya washiriki wapatao 3,600 kutoka mikoa yote Tanzania Bara wanatarajiwa kushiriki katika michezo ya UMITASHUMTA na washiriki 3,800 kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar watashiriki katika michezo ya UMISSETA,” amesema Shemdoe

Michezo itakayohusika ni mpira wa miguu, netiboli, mpira wa wavu, mpira wa mikono, mpira wa meza, riadha jumuishi, kwaya na ngoma na mpira wa kikapu.

Matangazo hayo yatakujia mbashara kupitia TBC1 na ukurasa wa YouTube wa TBCOnline.