Wanafunzi 150,000 wapangiwa sekondari na vyuo

0
259

Wanafunzi 153,219 wakiwemo wasichana 67,541 na wavulana 85,678, sawa na asilimia 91.8 ya wenye sifa, wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari Kidato cha Tano, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Elimu ya Ufundi mwaka 2022.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashingwa na kuongeza kuwa zoezi hilo limefanyika kwa kuzingatia takwimu za matokeo ya wanafunzi waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne Mwaka 2021 kutoka Tanzania Bara.

“Kati ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano, wapo wanafunzi wenye Mahitaji Maalum 48. Aidha, kati ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano, wanafunzi 41,401 watajiunga kusoma tahasusi za Sayansi na Hisabati na wanafunzi 49,133 watajiunga kusoma tahasusi za masomo ya Sanaa, Lugha na Biashara.

Kwa kuangalia takwimu za mwaka 2022, kumekuwa na ongezeko la wasichana 7,555 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi ukilinganisha na mwaka 2021.

Bashungwa ameeleza zaidi kuwa wanafunzi 14,254 wenye sifa ya kujiunga na kidato cha Tano wamekosa nafasi kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi waliofaulu na waliokuwa na sifa ya kujiunga na Kidato cha Tano na vyuo vya ufundi pamoja na ufinyu wa nafasi za Kidato cha Tano na Vyuo vya Elimu ya Ufundi (NACTVET).

“Wanafunzi hao wanatarajiwa kujiunga na kidato cha Tano katika awamu ya pili baada ya ukamilishaji wa baadhi ya miundombinu ya shule na vyuo,”amesema.