Wamiliki wa kumbi zinazopiga muziki kwa sauti kubwa waonywa

0
169

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewaonya wamiliki wa kumbi za starehe zilizo kwenye makazi ya watu zinazopiga muziki kwa sauti kubwa kinyume na maelekezo ya baraza hilo na kutaka kuacha kufanya hivyo.

Onyo hilo limetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt.Samuel Gwamaka na kubainisha kuwa licha ya elimu kuendelea kutolewa juu ya kelele na athari zake kwenye mazingira, baadhi ya wamiliki wa kumbi za starehe na nyumba za ibada bado wameendelea kukaidi sheria zilizowekwa.

“Sisi kama baraza tunaendelea kusimamia sheria za hifadhi na usimamizi wa mazingira ili kuhakikisha wananchi wanaishi kwa utulivu na amani kwenye maeneo yao, na hatutasita kuchukua hatua kali dhidi ya wote watakaoshindwa kufuata taratibu zilizowekwa.” amesema Dkt. Gwamaka

Amesema baadhi ya kumbi za starehe zimechukuliwa hatua kutokana na kupiga muziki kwa sauti kubwa na kuwataka watendaji wa serikali za mitaa kuendelea kushirikiana na NEMC ili kudhibiti hali hiyo.

Mpaka sasa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira limekamata vyombo mbalimbali vya wamiliki wa kumbi tatu za starehe katika wilaya za Temeke na Kinondoni mkoani Dar es Salaam, baada ya kushindwa kufuata sheria zilizowekwa na baraza hilo.