Wambura akiri makosa, aomba kusamehewa

0
169

Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), -Michael Wambura ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo jijini Dar es salaam kuwa, ameandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) kwa ajili ya kuomba msamaha na kukiri makosa yanayomkabili mahakamani hapo.

Wambura amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi,- Kelvin Mhina kuwa, ameandika barua hiyo kufuatia ushauri uliotolewa na Rais Magufuli kwa DPP, hivyo ameuomba upande wa mashitaka ufuatilie barua hiyo ili upate majibu kwa haraka.

Baada ya maelezo hayo, Wakili wa Serikali Wankyo Simon aliieleza Mahakama kuwa watafuatilia suala hilo ili wapate majibu mapema na kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 16 mwaka huu.

Wambura ambaye alikwishafungiwa maisha kujihusisha na soka, alifikishwa Mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 11 mwaka huu, akikabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi yenye mashitaka 17 yakiwemo ya kutakatisha fedha zaidi ya Shilingi Milioni Mia Moja.

Katika mashitaka hayo ya utakatishaji fedha, inadaiwa kuwa kati ya Agosti 15 na Oktoba 21 mwaka 2014 katika Makao Makuu ya TFF, Wambura alijipatia Shilingi Milioni 25 kutoka TFF huku akijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa la kughushi.

Pia, katika shitaka lingine la utakatishaji fedha, kati ya Machi 16 na Oktoba 21 mwaka 2015, anadaiwa kujipatia Shilingi Milioni 75.9 kutoka TFF wakati akijua kuwa fedha hizo siyo halali na zimetokana na shitaka la kughushi.