Waliotumia vibaya fedha za lishe kuwajibishwa

0
428

Rais Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa kuwachukulia hatua watendaji wote waliotumia vibaya fedha za lishe.

Rais ametoa agizo hilo mkoani Dodoma, wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa usimamizi wa shughuli za lishe.

Amesema hakubaliani na hatua ya watendaji kutumia fedha zinazotolewa kwa ajili ya lishe na kuzielekeza katika matumizi mengine.

Amesema kufanya hivyo ni utovu wa nidhani na wote waliofanya hivyo ni lazima wawajibishwe.

Pia Rais Samia Suluhu Hassan amewaagiza wakuu wa mikoa nchini kuhakikisha fedha kwa ajili ya miradi ya lishe zinatolewa kwa wakati.

Amewataka wasisubiri tu kupelekewa ripoti kuhusu lishe, bali watoke na kufuatilia kama fedha zilizotolewa zimetumika kama ilivyokusudiwa.

Kwa watafiti nchini, amewataka kufanya utafiti kuhusu lishe duni na matokeo yake yasambazwe nchi nzima ili kuondoa tatizo hilo.

Rais Samia ametaka utafiti huo pamoja na mambo mengine ujikite katika kuwasaidia vijana ambao ni wazazi watarajiwa.

Mkataba huo wa usimamizi wa shughuli za lishe umetiwa saini baina ya Rais Samia Suluhu Hassan na Wakuu wa mikoa ya Tanzania Bara.

Utiwaji saini wa mkataba huo umefanyika pamoja na tathmini ya sita kuhusu mkataba wa lishe uliosainiwa mwaka 2017.