Walioshindwa kukusanya mapato kutoa maelezo

0
2281

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo ameziagiza halmashauri zote nchini ambazo zimeshindwa kufikia malengo katika ukusanyaji wa mapato kutoa maelezo.

Waziri Jafo ametoa agizo hilo jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya hali ya ukusanyaji wa mapato katika halmashauri zote nchini kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018.

Amesisitiza kuwa wakuu wote wa mikoa nchini wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia ukusanyaji wa mapato na kuwataka kuzichukulia hatua halmashauri katika maeneo yao ambazo zimeshindwa kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato.

Waziri Jafo ameitaja mikoa ya Dodoma, Geita na Njombe kuwa ndio iliyovuka lengo katika ukusanyaji wa mapato huku mikoa ya Simiyu Ruvuma na Shinyanga ikifanya vibaya katika ukusanyaji wa mapato hayo.

Halmashauri 38 nchini nazo zimetajwa kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato, halmashauri ambazo ni pamoja na Geita, Kibaha, Bukoba, Temeke, Pangani na Kilombero.

Kishapu, Ilemela, Meru, Kyela na Iringa ni miongoni mwa halmashauri ambazo Waziri Jafo amesema kuwa zimeshindwa kufikia malengo katika ukusanyaji mapato.