Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amekabidhi taarifa ya uchunguzi wa mgogoro wa kijiji cha Mabwegere na vijiji saba vya wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro na kuagiza wote waliohusika kupotosha mipaka ya eneo hilo kuchukuliwa hatua za kisheria.
Waziri Lukuvi ametoa agizo hilo mkoani Morogoro wakati akikabidhi taarifa ya uchunguzi wa mgogoro huo kwa mkuu wa mkoa wa Morogoro Dkt Kebwe Stephen.
“Wote walioshiriki kwa namna moja ama nyingine katika process yote ambayo kwa kiasi fulani imeigharimu serikali fedha nyingi na kuipa maumivu serikali katika suala hilo ni lazima wachukuliwe hatua kali” amesema waziri Lukuvi.
Uchunguzi wa mgogoro huo uliofanywa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacob Mwambegele umebaini kuwa chanzo cha mgogoro huo ni kukosekana kwa ushirikishwaji wa vijiji jirani katika kuainisha na kuweka mipaka ya kijiji cha Mabwegere na hivyo kusababisha kijiji hicho kiwe na eneo lenye ukubwa wa hekta 10,234.
Hata hivyo Waziri Lukuvi amesema kuwa serikali haijakifuta kijiji cha Mabwegere bali ni kutekeleza taarifa ya uchunguzi ya kufuta mipaka ya kijiji hicho ambapo kwa sasa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na wilaya ya Kilosa itatakiwa kuanza mchakato wa kuandaa upya mipaka ya vijiji hivyo kwa njia shirikishi.
Katika taarifa yake, Jaji Mwambegere amependekeza kwa nia ya kuboresha utendaji kazi, weledi, maadili, umakini na uwezo wa kulinda na kutunza kumbukumbu katika idara ya upimaji na ramani na ofisi ya kamishna wa ardhi, hatua za kinidhamu zichukuliwe ili kuzuia migogoro ya ardhi.
Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Mendeleo ya Makazi ilikosea katika zoezi la upimaji kwa kuanzisha kijiji cha Mabwegere lakini wilaya ya Kilosa itakuwa na jukumu la kuanza mchakato upya wa upimaji katika vijiji hivyo.
Amesisitiza kuwa shughuli za binadamu kama vile ufugaji hazihusiani na masuala ya mipaka, hivyo wilaya ya Kilosa pamoja na kushughulikia suala la mipaka lazima iandae mpango wa matumizi bora ya ardhi na kuanza kupendekeza maeneo ya ufugaji kwa vijiji vyote saba na kwamba ni lazima busara itumike katika kushughulikia jambo hilo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Tamisemi, -Joseph Kakunda amesema kuwa uanzishwaji wa kijiji cha Mabwegere haukufuata sheria na kuwataka wataalamu kuacha kuwa na nidhamu ya woga na kuzingatia kanuni na sheria katika kutekeleza maj