Waliokimbia na Shilingi Bilioni 1.2 za Wakulima wasakwa

0
268

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani Mtwara kuwatafuta na kuwakamata viongozi wa vyama vya Msingi vya Ushirika, wanaotuhumiwa kukimbia na Shilingi Bilioni 1.2 za Wakulima ambazo ni madeni ya Korosho.

Mhandisi Masauni ametoa agizo hilo wakati akizungumza na Wakazi wa wilaya ya Newala mkoani Mtwara, wakati wa mkutano wa hadhara baada ya kupokea ripoti ya jumla ya madeni wanayodai Wakulima wa Korosho katika wilaya za Mtwara, Masasi, Nanyumbu, Newala na Tandahimba.

“Nilivyofika hapa Mtwara jambo la kwanza lilikuwa kumuuliza Kamanda wa Polisi wa hapa juu ya utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais alilolitoa siku za hivi karibuni alipofanya ziara, ambapo aliagiza kukamatwa kwa viongozi wawili wa vyama vya msingi vya Ushirika wanaodaiwa fedha za korosho na wakulima, ameniambia walitekeleza agizo na hao viongozi  wawili tayari wameanza kulipa hizo fedha,” amesema Naibu Waziri Masauni.

Akizungumza baada ya kupokea ripoti ya madeni kwa wilaya zote za mkoa wa Mtwara, Naibu Waziri Masauni amelitaka Jeshi la Polisi mkoani humo kuwakamata viongozi wengine katika wilaya zilizobaki za Mtwara, Newala, Masasi, Nanyumbu na Tandahimba ambapo katika ripoti hiyo inaonyesha takribani Shilingi Bilioni 1.2 bado zinadaiwa na wakulima hao wa Korosho kutoka kwa viongozi wa vyama hivyo vya Msingi vya Ushirika.

“Mheshimiwa Rais kwenye ziara yake aliishia wilaya ya Masasi, lakini katika ripoti hapa inaonyesha katika wilaya zingine Wakulima pia wanadai fedha zao ambazo ni kiasi kikubwa, nakuagiza Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara kuwakamata viongozi wengine katika wilaya zilizobaki na hakikisha fedha za wakulima hao zinalipwa,” ameongeza Naibu Waziri Masauni.

Katika ripoti yake aliyoisoma kwa Naibu Waziri Masauni, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mtwara, – Blasius Chitanda amesema kuwa, zaidi ya Vyama vya Ushirika Sitini bado vinadaiwa na Wakulima katika wilaya za Mtwara, Masasi, Tandahimba na Newala, madai ambayo ni kuanzia msimu wa Korosho wa mwaka 2015/2016 hadi mwaka 2017/2018.