Waliojichukulia sheria mkononi waachiwa kwa agizo la RC

0
170

Jeshi la polisi mkoani Geita limewaachia watu kadhaa waliokuwa wakishikiliwa katika kituo cha polisi cha Buseresere wilayani Chato mkoani Geita, kwa tuhuma za kujichukulia sheria mkononi baada  ya mwanafunzi wa kidato cha pili wa shule ya sekondari ya Buseresere Suzana Lubuga kugongwa na basi na kufariki dunia katika eneo hilo. 
 
Watu hao ambao ni wanafunzi watano na walimu watano wa shule ya  sekondari ya Buseresere pamoja na wakazi wengine saba wa eneo hilo walikuwa wakituhumiwa kwa kufunga barabara na kufanya uharibifu wa mali, na wameachiwa na polisi kufuatia agizo la mkuu wa mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule.

Akizungumza na walimu na wanafunzi wa shule hiyo ya sekondari ya Buseresere, Senyamule amewataka kutojichukulia sheria mkononi pindi panapotokea tatizo lolote na badala yake wafuate utaratibu wanapotaka kuwasilisha malalamiko yao.
 
Nao wanafunzi wa shule hiyo ya sekondari ya Buseresere wameziomba mamlaka husika kuongeza alama za barabarani katika eneo wanalovukia na kuendelea kuwapatia elimu ya usalama wa barabarani.
 
Dereva wa basi lililomgonga mwanafunzi huyo ambalo ni mali ya  kampuni ya FIKOSHI lililokuwa linafanya safari zake kutoka Bukoba mkoani Kagera  kuelekea mkoani Mwanza wakati ajali hiyo inatokea, bado anashikiliwa na polisi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani.