Waliojenga ukuta Mirerani kupatiwa ajira

0
182

Vijana 2,033 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) walioshiriki kwenye ujenzi wa ukuta katika machimbo ya madini ya Tanzanite huko Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wametakiwa kufika kambi ya JKT Mgulani iliyopo jijini Dar es salaam tarehe 12 mwezi huu kwa ajili ya mchakato wa kupatiwa ajira

Tangazo hilo limetolewa jijini Dar es salaam na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo, wakati wa mkutano wake na Waandishi wa habari.

Jenerali Mabeyo pia ametangaza mabadiliko yaliyofanywa na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Rais John Magufuli, ambapo Brigedia Jenerali
Charles Mbuge anakuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa na aliyekuwa Mkuu wa JKT Meja Jenerali Martin Busungu anakuwa Mkuu wa Jeshi la Akiba.

Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo, ametumia mkutano wake na Waandishi wa habari, kuwataka Watanzania wote hasa vijana wanaopitia mafunzo ya JKT kuondoa dhana ya kuwa ni lazima wapate ajira Jeshini.

Amesisitiza kuwa hakuna kijana aliyepitia mafunzo ya JKT ambaye amewahi kuhusika kwenye matukio ya uhalifu kama inavyoelezwa na baadhi ya watu.