Waliogomea wito wa Dkt. Mollel watakiwa kujieleza

0
188

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewaagiza wakandarasi kutoka kampuni ya Luba, MUST na Ardhi ambao waligomea wito wake wa kuwataka wafike katika eneo la mradi wa ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida, kufika kwa mkuu wa mkoa huo ili wajieleze kwa nini mradi huo haujamalizika ndani ya wakati licha ya kulipwa fedha zote na Serikali.

Dkt. Mollel ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida pamoja na kukagua hali ya utoaji huduma katika hospitali hiyo.

Amesema wakandarasi kutoka kampuni ya Luba, MUST na Ardhi wamegoma kufika eneo la ujenzi, licha ya yeye kutoa maelekezo wawepo ili kujadili changamoto zinazowafanya kushindwa kutekeleza makubaliano ya kumaliza mradi huo ndani ya muda uliopangwa.

Kwa mujibu wa Dkt. Mollel, mkandarasi kutoka Luba alitakiwa kumaliza kazi mwezi Julai mwaka 2022 lakini hakutimiza makubaliano hayo licha ya kuongezewa muda mpaka mwezi Novemba mwaka huo huo wa 2022, huku Serikali ikiwa imetimiza jukumu lake la kutoa kiasi chote cha fedha kwa ajili ya mradi huo.

Akiwa mkoani Singida, Dkt. Mollel pia amewataka watendaji wa
hospitali ya Rufaa ya mkoa huo kuongeza juhudi katika utoaji huduma.