Waliobishania vipimo wasimamishwa kazi

0
165

Serikali imewasimamisha kazi watumishi wawili wa afya wa zahanati ya Ishihimulwa iliyopo kwenye halmashauri ya Uyui mkoani Tabora, baada ya kukutwa na makosa katika picha ya video iliyowaonesha wakibishana kuhusu namna ya kutoa huduma kwa wagonjwa.

Watumishi hao Rose Shirima ambaye ni muuguzi mkunga na James Chuchu ambaye ni mteknolojia wa maabara, tarehe 6 mwezi huu walionekana kwenye video hiyo wakibishana kuhusu matumizi ya vifaa vya kupimia Malaria (MRDT) kama vimekwisha muda wake au la.

Kutokana na tukio hilo, wizara ya Afya, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na halmashauri ya Uyui walianzisha uchunguzi wa tukio hilo na kuwakuta watumishi hao na makosa ya kinidhamu kazini.